Tuesday, June 9, 2015

Mulenda: Kipaumbele ni elimu bora

Bw. Leonce Mulenda

Mulenda (41) amechukua fomu ya kuwania kuteuliwa na chama chake kugombea urais huku akisema kipaumbele chake cha kwanza ni elimu bora.

Kada huyo ambaye alisindikizwa na watu wasiozidi sita, alisema kaulimbiu yake ni Serikali sikivu, makini na inayojali shida za watu.

Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo katika ofisi za Makao Makuu ya CCM, Mulenda alisema amejitathmini na kujipima kuwa anaweza kuwa kiongozi wa Tanzania. 

Alitaja vipaumbele vingine kuwa ni kuhakikisha CCM inakuwa imara zaidi.
“Kwa upande wa chama nitahakikisha nasimamia kwa vitendo katiba ya chama, kanuni na taratibu bila kuacha sheria na miongozo inayoongoza nchi yetu,” alisema.

Alisema atasimamia uamuzi wa vikao na kuhakikisha unatekelezwa na kupima matokeo kwa kufanya tathmini juu ya malengo waliyojiwekea.

Mulenda alisema endapo atashinda na CCM ikawa ndicho chama tawala, atakuwa na kazi ya kuisimamia Serikali.

“Ukiona Serikali inafanya vibaya na chama kinachotawala kinaona sawasawa, basi siku za kukaa madarakani za chama hicho zinahesabika,” alisema.

Alisema endapo atafanikiwa katika safari yake hiyo, atahakikisha Serikali yake kupitia ilani ya uchaguzi ya CCM inakuwa sikivu, makini na inayojali shida za watu.

“Nawahakikishia wananchi kuwa kwa kutambua shida zao ni dhahiri nitajua wanataka nini na hawataki nini na kwa msingi huo, Serikali itakayokuwa chini yangu wakati wote tunahakikisha Watanzania tunawapeleka kule wanakotarajia kwa kutumia uwezo wetu ambao ulijengwa na waasisi wa Taifa hili,” alisema.

Alisema wazee waliwaambia kuwa nchi ina raslimali za kutosha na kinachotakiwa ni kujiongoza ili kutumia amani na utulivu kujenga nchi.

0 comments:

Post a Comment